Birthdays

MT's Third Birthday
Heri ya siku yako ya kuzaliwa MT, miaka mitatu sasa duniani na naamini MUNGU atatusaidia tuendelee kuihesabu kwa mamoja na makumi tele.
Ilikuwa mara yangu ya pili kuingia "leba" na mama yako, (mara ya pili kwa mama yako pia ).... tayari tulishaandaa majina, moja la kike na moja la kiume, mama ni mama tu, alishajua kuwa utazaliwa wewe na kweli ukazaliwa wewe tukakuita Marytheresa, jina la mama mkwe wangu kipenzi na kufanya family yetu kuwa na watoto wenye majina ya mama zetu wote.
Nilikupenda kabla hata ya kutungwa kwa mimba yako, hakuna kingine zaidi ya kumpenda mtu ambaye ni kiini cha upendo wenyewe, wewe hapo mwanangu na kama waona hautoshi huu upendo niambie "niuongeze sauti". Maisha yamefanya tuwe mbali na mama yako, hatulipendi hili na tunajitahidi kulirekebisha, hii inanifanya niwe baba na mama kwako kwa wakati mmoja ili usijihisi kupungukiwa, nashukuru MUNGU angalau hili linamudika japo ukweli ni kuwa bado tunamuhitaji sana mama yako, tusamehe mwanangu ila fahamu uko salama nami, mama yako kuniamini kiasi cha kuniacha nawe kunadhihirisha "usalimini".
Wewe ni nguvu na uwezo wangu, sikujua kwamba mimi ni Mwanasaikolojia, Daktari, Bingwa wa mahesabu na vingine vingi mpaka pale nilipoongeza ukaribu ktk kukulea, ukaribu unaonifanya kuwa sehemu kuu ya maisha yako, ukaribu wa si tu kutoa hela ya chakula bali kukupikia na kukulisha kwa mikono yangu, ukaribu wa kujua muda gani na mara ngapi nikuamshe usiku ili usikiloweshe kitanda, ukaribu wa kujua cheko lako lipi ni la furaha yako kuu.
Babaako nimekuwa sio mzuri sana when it comes to ahadi, nimewaangusha baadhi ya watu nikiwamo mimi mwenyewe, wajua nabaki kuwa binadamu kama binadamu wengine...lakini sitaki hii iwe excuse, NAKUAHIDI na wala siogopi kukuahidi kutimiza ahadi zote nilizojiahidi mimi na mama yako kuhusu wewe, MUNGU na atusaidie sana.
Nafurahi unajua vitu vingi kabla hata hujaanza shule, nitambue mchango wa dadaako KITA kwa uwezo ulionao, amekuwa mwalimu mzuri kwako, good news ni kwamba Vile vilio vyako vya kutaka kuongozana na Kita kwenda shule kila asuhuhi apandapo gari, leo vinafikia kikomo....Hii najua ndio zawadi utakayoipenda sana, kwamba kuanzia

JUMATATU UTAVAA UNIFORM KWENDA SHULE NA KITA
Wynjones Kinye
August 12 at 10:14am





Kita's Fifth Birthday


Happy 5th Birthday Lizbeth-Kita.
Umeendelea kuwa baraka kwetu na tunajivunia sana mwanangu, pia umeendelea kuwa sababu ya sisi wazazi wako kuendelea kuimarika, kuzidi kupendana, na kutupa hamasa ya kupambana na maisha...ni magumu lakini tunayamudu kwani tulishaahidi kutokukuangusha kwa namna yoyote.
Leo umetimiza miaka mitano, unanifanya nikumbuke makubwa yaliyokutokea kwenye mwaka wako wa nne....hata ukija kusoma hichi nachoandika miaka ijayo basi tambua kuwa ni kwenye mwaka wako wa nne umeweza kuandika jina lako, jina la mama yako, jina la mdogo wako na bado unajitahidi kuweza kulimudu langu (nilipewa jina gumu sana kwakweli hivyo nakuvumilia)...pia umemudu kudhihirisha ukali wako kwenye hesabu, mama yako ni mkali sana wa hesabu ila moto wako unaunguza zaidi...endelea hivyohivyo mpaka kuufikia ubingwa. Umeweza kusoma "sounds", "words", na sasa unaunganisha "sentence"...najivunia sana wewe kwakweli. Unanishangaza sana kwa uwezo wako kimasomo, unajua vitu mpaka wakati mwingine natazamana na mama yako na kuanza kucheka (kuashiria kuwa unachojua sasa sisi tulikijua tukiwa wakubwa kidogo)....nilipokea habari nzuri kutoka kwa mwalimu wako kuwa mwakani "utarushwa" darasa kwakuwa unaelewa haraka na vikikaa vimekaa kichwani...nazidi kujivunia wewe, nitaendelea kuwa nawe karibu wakati wote wa kusoma kwako, tutafanya homeworks pamoja kwa miaka mingi sana. Kwa mafanikio yako haya mimi nawashukuru na ukikua utambue mchango wa waalimu wako Teacher Clara na Teacher Getrude, wanajitahidi sana kwakweli na nawashukuru sana. Pia aunt Dora ni wa kushukuriwa sana kwa juhudi zake za kukupelekea chakula shuleni kila siku ili ushibe na kupata nguvu ya kusoma, anaonyesha kukupenda sana kwakweli.
Umekuwa dada mzuri kwa MT na zaidi umekuwa mwalimu wake, tazama leo MT ana count to ten pasi kwenda shule, tazama leo MT anaimba sounds pasi kwenda shule na vingine vingi wamfunza, endelea hivyohivo, ukue ukijua kuna mdogo wako anahitaji uwepo wako katika kila kitu, shikamana naye kila siku pasi kuschoka.
Naendelea kumshukuru mamaako Agatha Nicholaus kwa malezi na upendo, kwake mimi na wewe ni watoto japo kwako mimi ni baba, amejitoa sana kwa ajili yetu, natamani ukue ukiiga matendo mazuri ya moyo wake na zaidi maadili.
Tunatazamia makubwa sana kwenye mwaka wako wa tano kadri Mungu atakavyotujaalia, tutakoleza zaidi upendo wetu kwako, tutaongeza zaidi ukaribu wetu kwako, tutaongeza zaidi muda na wewe ili kwa namna yoyote msingi tulioanza kuujenga kwako uzidi kuwa imara. Tunajinyima kukuridhisha….si tu kwa vile unavyohitaji bali kukuridhisha pia kwa vile tunavyohitaji sisi kwako, tunawekaza pia kwa futere yako na mdogo wako, sala zako kila siku kabla hujafunga macho yako kwakweli zinajibiwa vizuri na Mungu wetu tunayemwamini, kwa mapenzi yake Christmass hii utailia chini ya paa la jasho la wazazi wako…sehemu ambayo ndio utasema rasmi kuwa ni nyumbani, sehemu ambayo ni urithi wenu tukiwa hai na hata ikatokea tumetangulia mbele ya haki…husemwa ukiwa kwako hata ukila dagaa kila siku haihusu, ni kweli lakini nataka nikuhakikishie kuwa tutahakikisha kuwa utakula sausage, dagaa ule kwa kupenda na si kuwa imelazimu
(Eee Mungu utusaidie).
Nakuombea kila zuri duniani na mbinguni, nafurahi kuona kila hatua ya ukuaji wako kuanzia unatoa kichwa na kulia kwa mara ya kwanza mpaka sasa umetimiza miaka mitano. Endelea kuwa rafiki yangu wa karibu, rafiki pekee ambaye sina hofu ya kuumizwa naye, rafiki ninayeamini kuwa nikilia atalia nami huku akinifuta machozi, nitautakasa moyo wako wa dhahabu, nitaka kuyashuhudia maisha yako ya upendo na furaha.
NAKUPENDA KITA, NAKUPENDA LIZBETH…HAPPY BIRTHDAY.


Kita's Fourth Birthday
Nakosa pa kuanzia...siku yako hii Lizbeth "kita" (sababu yangu nyingine ya kufurahi).
Unajua mara kadhaa watu na dunia vimeniudhi na kufanya niikunje sura yangu nzuri, ila haijawahi tokea niingie na sura hiyo nyumbani ulipo, nikikuona tu nafurahi, unikimbiliapo na kunirukia nafurahi zaidi, kabla ya salamu unavyonilipua na busu ndio kabisaaaaaaa shida natupa kule.
Nafurahia uwepo wako kila siku, hata sichoki kuwa pembeni yako, hainikeri kuchoma mafuta kila siku saa sita kamili kukuchukua shule na kukurudisha nyumbani, na nichelewapo kukufuata nawehuka...hutamani niyapandie kwa juu magari barabarani.
Mwaka wako wa nne huu tumeusherehekea ukiwa shuleni, ukiwa na classmates na waalimu wako wanaojupenda sana, mimi na mamaako tumeifurahia sana siku, japo tumesherehekea kwa dk 45 tu lakini kuuona uso wako ukiwa na furaha ile kumeturidhisha sana mwanangu, tutajitahidi uwe hivyo kila siku.
Wengi wanashiriki nasi kukupenda, kukujali na kufanya uwe ulivyo, naamini utakua ukihifadhi haya tukupayo katika sehemu nzuri ya moyo wako, umekua umeenda shule...tunasubiri siku upike tule.
Nakusifu kwa kuwa dada mzuri kwa mdogo wako Mary, kwa kumchangamsha na kumpa muongozo katika mambo yamfaayo, endelea kuwa hivi hata miaka itakapozidi kwenda. Mwalimu wako "teacher clara" amekusifu kuwa una upendo sana kwa watoto wadogo shuleni, sifa hizi zimenivimbisha bichwa kweli huku nikijivunia moyoni kuwa kumbe hauko ulivyo kwa mdogo wako tu, bali kwa kila mmoja...endelea kuwa hivyo mwanangu.
Safari yako ya kuingia mwaka huu wa nne imekuwa nzuri sana, ni mwaka ambao umewajua ndugu zako wengi wa upande wa mama na wa baba, wa mjini na kijijini...ni mwaka ninaouzingatia kama uliolipa deni kubwa...deni la mabibi na mababu, mashangazi na wajomba, wamama na wababa na binamu zako kukujua....safari ya april hadi may ilitimiza yote haya. Sijui ni lini tena tutawaona tuliowaona lakini najua kuwa unatakiwa kuwa karibu na ndugu zako, nitakukuza nikiwa nakukumbusha umuhimu wa kuwa karibu na nduguzo.
Nakushukuru kwa nguvu unayonipa...nguvu ya kupambana usiku na mchana...kutwa na wakati mwingine kuchwa, nakuahidi kuwa mpambanaji ili kuzitimiza ndoto zangu zinazokuhusu, wakati utafika na haya nisemayo yatadhihirika.
Napenda utamaduni wako wa kusali kabla hujalala, endelea hivyohivyo, Mungu ni wa kutangulizwa popote, hata ile Biblia unayolala nayo ni yako, tutaitunza hadi ufike wakati wa wewe kuisoma mwenyewe.
Kumbukumbu yako ni kumbukumbu ya mamaako pia...mke wangu, mhimili wa familia yetu, shujaa wa ukweli, nilishuhudia akipambana na kukuleta duniani, alilia sana lakini mara tu baada ya wewe kulia alibadilika na kuanza kufurahi, mimi naye tukalia tena sana kwa furaha huku ukiwa huelewielewi nini kinachoendelea...nampenda na kumheshimu sana mamaako, nisaidie nawe kumpenda na kumheshimu siku zote za maisha yako, msikilize na kumtii.
Niitumie siku hii kuwashukuru aunt zako aisha na dorah (wasaidizi wetu pale nyumbani)...hakika wamekuwa msaada mkubwa sana kwetu ktk kukulea pindi sisi tuwapo mihangaikoni.
Iwe kwenye kumbukumbu yako kuwa cake yako hii ya nne imewezeshwa na ankal lako @nourchriss kama alivyokuahidi...Huyu Mimi na mamaako no wasimamizi wa ndoa yake na @neyruge ....jiandae kuwa msisimamizi wa watoto wao pindi watakapozaliwa .
Love you my lizbeth "kita"

Wynjones Kinye
November 7, 2014 ·

MT's Second Birthday
Heshima na utukufu kwako ee Mungu kwa kutukuzia zawadi hii yako kwetu, malaika wetu...furaha yetu...sababu yetu ya kuimarika...binti yetu MT...it's her 2nd birthday (ona siku zinavyokimbia).
Dear MT,
mimi na mama yako tulimuomba Mungu wewe akatupatia wewe...wewe ni jibu la maombi yetu na kila siku tunayojaaliwa kuiona ni ya kumshukuru Mungu kwa wewe...kwa moyo wa dhahabu kama wa dada yako niseme kuwa umekuwa "mwenza" mzuri sana wa Kita, naona jinsi mnavyouimarisha umoja wenu kila siku nasi tunajivunia sana.
Kama baba unanihamasisha sana kupigana, sijui nimeshinda mapambano mangapi kwa ajili yako...ni mengi na kamwe sitohesabu kwani ni jukumu langu kwako, kitokacho kwangu si kitu zaidi ya kiingiacho kwako....akili na nguvu zangu ni kwa ajili ya furaha na mahitaji yako...of course na moyo na roho yangu ni kwa kukupenda na kukufurahia.
Kwa miaka miwili hii tayari umeshaonyesha dalili zoote nzuri za kuwa mtoto mwema kwetu na mtu mwema kwako wewe mwenyewe...kama mzazi nitahakikisha hubadiliki...usikivu wako kama mtoto endelea nao siku zote za maisha yako...ni kutoka usikivuni utavumbua na kugundua visivyoonwa....upendo wako kwetu na kwa wanaokuzunguka pia endelea nao, naona pia unavojipenda wewe mwenyewe (muhimu sana mwanangu)...ila unanivutia unavyojipenda pasipo kujipendelea...najivunia vitu hivi na vingine vingi ulivyonavyo ndani yako...vinaongeza sana thamani yako kama binadamu, leo nakuambia hivi ni salaha muhimu kwako kuyakabili maisha zaidi ya uzuri ulionao (wewe ni mzuri sana mwanangu).
Umemaliza mwaka wako wa kwanza na sindano...malaria imekutesa kweli...umepungua kilo kadhaa, cha kumshukuru Mungu ni kuwa unauanza mwaka mpya ukiwa na afya...tabasamu lako asubuhi ya leo baada ya kukupa busu la birthday ni uthibitisho mkubwa...na hata uliponikumbatia nikahisi joto lako kuwa normal tofauti na jana na juzi....tunamshukuru Mungu na ufundi wa daktari ktk kupigania afya yako.
Mwakani nawe utaanza shule, uko tayari kabisa mwanangu...naona jinsi nawe unavyoshughulika pindi Kita afanyapo assignments zake, jinsi unavyorudia numbers..sounds...na alphabets anazoimba...hata siku ulipoingia darasani kwa Kita ulifurahi kwa namna ya kipekee...kwa furaha nilifuta "kachozi"
Siwezi weka nukta pasipo kumshukuru mamaako Agatha Nicholaus kwa ajili yako...kwa ajili yenu...kwa ajili yangu...kwa ajili yetu. Amekuwa muhimili mkubwa na muhimu sana wa familia yetu, tumpende kumtia nguvu zaidi...tumuheshimu na kumlinda asikate tamaa....nyie ni nguvu yangu...nawapenda sana.
HAPPY BIRTHDAY MT




MT's First Birthday
Happy Birthday Baby MT....ya kwanza hii mwanangu na veeeerrrrrry maalum, niseme nini babaako zaidi ya kumshukuru Mungu aliye juu kwa zawadi hii ya ghali mno?!! Hivi wajua navyojisikia kushuhudia ukuaji wako siku baada ya siku...? Kwakweli ni zaidi ya kumilikishwa dunia, ni nusu ya kuwa peponi.
Nilikuwa pale wakati shujaa mamaako akikuleta duniani (nani kama mama?)...nililia alipolia kwa maumivu, ulipotoka tu na kulia kwa mara ya kwanza mimi na yeye tukalia zaidi huku tukitabasamu...kilo 3.7 alizitoa kijasiri. Unajua sauti yako baada ya kulia ilizungumza maneno mengi sana?!! Sauti ile ilimaanisha vingi sana kwetu (nitakuambia siku moja), mimi na mamaako tulitazamana tukiwa tumeshikana mikono kwa nguvu sana tukasali kumshukuru na kumsifu Mungu kwa zawadi wewe...tulikwisha kuandalia jina mwaya...tukaanza kujulisha watu kuwa Marytheresa kazaliwa.
Umeongeza baraka kwenye nyumba yetu, umekoleza utamu kwenye ndoa yetu, umempa heshima ya cheo Kita...eti naye ni dada!! Anajidai sana na tunawaangalia na kufurahi sana kila siku. Natamani kuwaona mkikua pamoja mngali na upendo mlio nao kwa kila mmoja, sisi tunajitahidi na tutajitahidi kuwatengenezea maisha mazuri, si yale sisi wazazi wenu tuliyopitia...hayakuwa mabaya lakini kuna viwili vitatu hatutopenda mviexperience.
Nakuombea kwa Mungu ukue salama ukiwa mwenye afya tele, kwanini tusimshukuru Mungu ikiwa gonjwa kubwa lililowahi kukupata wewe ni mafua na kikohozi?? Sifa na Utukufu kwako ee Yesu. Nazidi kukuombea mwaka huu wa kwanza kuwa mwanzo wa safari yako ya uzeeni, ufike kule ukiwa mwenye busara na vingi vya kutoa kwa watu wenye uhitaji na wasio na uhitaji, uwe majibu ya maswali yaliyoshindikana duniani huku ukitembea katika njia inayompendeza Mungu baba yetu.
TUNAKUPENDA MT, ISHI MINGI.
Dad.


Kita's Third Birthday

Happy Birthday Lizbeth Wynjones "KITA".
Bado watufanya tujisikie kama tulivyojisikia miaka mingine iliyopita, kila siku kwa upya wake. Umekua sana hivi sasa, twaongea, twacheka, twafurahi tukiwa na sababu inayoeleweka kufanya hivyo, umeipamba nyumba na kuiipa heshima kuu, hata hivi sasa ikiwa na mgeni mpya bado umeimudu na kuwa mwenyeji mzuri wa Marytheresa.
Endelea kumlea, endelea kuwa mtetezi wake, endelea kuwa dada mzuri kwake...naamini mtakuwa marafiki licha ya undugu wenu wa damu.
Nna mengi ya kukuambia, raha ya mwaka huu ni kuwa umesikia na kuelewa kile tulichoongea asubuhi kitandani baada ya wewe kuamka nami kukuimbia na kukuombea kabla sijatoka kwenda kazini, jioni nitakuambia mengine tukiwa tunapiga picha, tahifadhi kumbukumbu hiyo pia.
Sasa una kila sababu ya kwenda shule, sehemu ambayo umekuwa ukiitaja mara kwa mara, jana nimepita pale jirani na nyumbani na wakaniambia cha kufanya...ndani ya mwezi wako huu wa kuzaliwa utavaa sare na kuhudhuria madarasa, umekua sana mwanangu.
Bado nakazana na haya maisha, si mepesi lakini naahidi kuhakikisha yanakuwa. Nakumbuka kukuahidi mengi, na leo nakuahidi kuyatekeleza yote na mengine yatakayobebana na yatakayolazimika ama kutamanika kutekelezwa.
Love you.
Daddy.





Kita's Second Birthday
Kita at two
umezaliwa tena 'KITAWETU' na hii ni barua ya pili kwako.
Mwaka jana tar ya leo nilikueleza mengi ikiwa ni pamoja furaha uliyoipanda kwenye mioyo yetu! Mwaka huu nafurahi zaidi na kifua kikiwa mbele nafurahi kukuambia kwamba tayari mimi na mama yako Agatha Nicholaus tu mume na mke hivyo wewe na sisi ni familia iliyo kamili sasa na yevye baraka na vibali vyote toka kwa Mungu na Wazazi.
Bado tuna ndoto kubwa kwako, nyingine binafsi sijui zitatimiaje lakini zitatimia tu kwa sababu tunaishi.
Bado wewe ni pambo la nyumba yetu na mioyo yetu, wazipa tabasamu nyuso zetu hata pale maisha yanapotupiga, kwa ajili yako tunasimama na kusonga mbele.
Bado watupa thamani kama wazazi, bado watupa ujasiri, bado watutia nguvu ya kusema hili na hili tutalifanya.
Najua bado sijawa baba ambaye mimi mwenyewe nataka niwe kwako, hii inaniumiza lakini kuwa mvumilivu mwanangu...kule upareni twasema "gumirija vyedi vyedhie" yaani vumilia vizuri vyaja, nilishaahidi kuwa hutaishi maisha niliyoishi mimi, hutasoma shule nilizosoma mimi, hutapambana na daladala ama kutembea umbali mrefu kwenda shule.
KITA! Una booonge la mama, najua u mdogo lakini unaenjoy upendo wake kwako, zaidi unaona ama kuhisi namna anavyojitoa kwa familia, ni bahati kubwa kuwa naye kama MKE na kuwa nawe kama MTOTO, kua uendelee kuliona hili ili ujifunze ayafanyayo hata uyafanye muda wako ukiwadia.
Upendo mwingi umekuzunguka Kita! Ndugu, Marafiki, Majirani na kila mtu amekuongelea vizuri...hili linatosha kukupa ulinzi wa furaha, naamini upendo huu utaendelea kukuzunguka kadri uongezavyo miaka, usiharibu hapo katikati, sawa mama?
Nina mengi ya kusema Kita, hata nikipewa siku nzima sitayamaliza hapa...nifupishe tu kwa kusema NAKUPENDA SANA, NAKUJALI SANA, na NAOTA MENGI KUKUHUSU.
Baba.



Kita's first Birthday
 

 

HAPPY BIRTHDAY KITA.

Wewe ni Tulizo na Amani yangu Rohoni,
Maisha ya Furaha ndiyo nikutakiayo Duniani,
Nakuombea Moyo wa Dhahabu uimarishe yako Thamani,
Hakika Ujio wako umebadilisha maisha yetu "yangu na ya mamaako"
Umetukuza kifikra na kutuweka pamoja zaidi,
Umetufanya tujue kuwajibika ili ule na kuvaa,
Umetupa heshima kwa ndugu na jamaa,
Umetupa hadhi na imani za wadau Wanaotuzunguka.
Tazama umetufanya kuwa Familia,
Hujui tu nilivyojickia nilipokusikia unalia,
Nilikuwa pembeni ya mamaako wakati anakutoa,
Picha nakutunzia, utaziona Utakapokuwa.
Mamaako ni jasiri sana...mwanamke wa kipekee kabisa katika dunia ya sasa,
Nampenda na kumuheshimu sana.
Umechukua jina la mamaangu mzazi..LIZBETH,
Angekuwepo angefurahi sana,
Naamini huko alipo anatabasamu kama kawaida yake,
Yeye ni Malaika mwingine,
Nitakueleza mengi kuhusu yeye ukianza shule.
Nakuwazia maisha imara hapo baadae utakapokuwa mkubwa,
Wakati ni huu kuyatengeneza ukiwa bado mdogo,
HII NI AHADI KUU KABISA "kwamba nitahakikisha unakuwa mwanamke imara wa kujitegemea, kujiamini na mwenye upendo kwa watu.
Wewe ni WIMBO nisiochoka kuusikiliza,
kwakuwa umetengenezwa vizuri na kuimbwa kwa sauti imara...
Ona macho yako!! Mamaako anafurahi kwakuwa yanafanana na yangu japo nakiri umenizidi kidogo.
HAPPY BIRTHDAY TO YOU LIZBETH WYNJONES ..."kita"...DADY LOVES YOU SO MUCH.