Thursday 8 September 2016

KITA'S FOURTH BIRTHDAY

Nakosa pa kuanzia...siku yako hii Lizbeth "kita" (sababu yangu nyingine ya kufurahi).
Unajua mara kadhaa watu na dunia vimeniudhi na kufanya niikunje sura yangu nzuri, ila haijawahi tokea niingie na sura hiyo nyumbani ulipo, nikikuona tu nafurahi, unikimbiliapo na kunirukia nafurahi zaidi, kabla ya salamu unavyonilipua na busu ndio kabisaaaaaaa shida natupa kule.

Nafurahia uwepo wako kila siku, hata sichoki kuwa pembeni yako, hainikeri kuchoma mafuta kila siku saa sita kamili kukuchukua shule na kukurudisha nyumbani, na nichelewapo kukufuata nawehuka...hutamani niyapandie kwa juu magari barabarani.
Mwaka wako wa nne huu tumeusherehekea ukiwa shuleni, ukiwa na classmates na waalimu wako wanaojupenda sana, mimi na mamaako tumeifurahia sana siku, japo tumesherehekea kwa dk 45 tu lakini kuuona uso wako ukiwa na furaha ile kumeturidhisha sana mwanangu, tutajitahidi uwe hivyo kila siku.
Wengi wanashiriki nasi kukupenda, kukujali na kufanya uwe ulivyo, naamini utakua ukihifadhi haya tukupayo katika sehemu nzuri ya moyo wako, umekua umeenda shule...tunasubiri siku upike tule.
Nakusifu kwa kuwa dada mzuri kwa mdogo wako Mary, kwa kumchangamsha na kumpa muongozo katika mambo yamfaayo, endelea kuwa hivi hata miaka itakapozidi kwenda. Mwalimu wako "teacher clara" amekusifu kuwa una upendo sana kwa watoto wadogo shuleni, sifa hizi zimenivimbisha bichwa kweli huku nikijivunia moyoni kuwa kumbe hauko ulivyo kwa mdogo wako tu, bali kwa kila mmoja...endelea kuwa hivyo mwanangu.
Safari yako ya kuingia mwaka huu wa nne imekuwa nzuri sana, ni mwaka ambao umewajua ndugu zako wengi wa upande wa mama na wa baba, wa mjini na kijijini...ni mwaka ninaouzingatia kama uliolipa deni kubwa...deni la mabibi na mababu, mashangazi na wajomba, wamama na wababa na binamu zako kukujua....safari ya april hadi may ilitimiza yote haya. Sijui ni lini tena tutawaona tuliowaona lakini najua kuwa unatakiwa kuwa karibu na ndugu zako, nitakukuza nikiwa nakukumbusha umuhimu wa kuwa karibu na nduguzo.
Nakushukuru kwa nguvu unayonipa...nguvu ya kupambana usiku na mchana...kutwa na wakati mwingine kuchwa, nakuahidi kuwa mpambanaji ili kuzitimiza ndoto zangu zinazokuhusu, wakati utafika na haya nisemayo yatadhihirika.
Napenda utamaduni wako wa kusali kabla hujalala, endelea hivyohivyo, Mungu ni wa kutangulizwa popote, hata ile Biblia unayolala nayo ni yako, tutaitunza hadi ufike wakati wa wewe kuisoma mwenyewe.
Kumbukumbu yako ni kumbukumbu ya mamaako pia...mke wangu, mhimili wa familia yetu, shujaa wa ukweli, nilishuhudia akipambana na kukuleta duniani, alilia sana lakini mara tu baada ya wewe kulia alibadilika na kuanza kufurahi, mimi naye tukalia tena sana kwa furaha huku ukiwa huelewielewi nini kinachoendelea...nampenda na kumheshimu sana mamaako, nisaidie nawe kumpenda na kumheshimu siku zote za maisha yako, msikilize na kumtii.
Niitumie siku hii kuwashukuru aunt zako aisha na dorah (wasaidizi wetu pale nyumbani)...hakika wamekuwa msaada mkubwa sana kwetu ktk kukulea pindi sisi tuwapo mihangaikoni.
Iwe kwenye kumbukumbu yako kuwa cake yako hii ya nne imewezeshwa na ankal lako @nourchriss kama alivyokuahidi...Huyu Mimi na mamaako no wasimamizi wa ndoa yake na @neyruge ....jiandae kuwa msisimamizi wa watoto wao pindi watakapozaliwa .
Love you my lizbeth "kita"

Wynjones Kinye
November 7, 2014 ·